Watu wawili wamefariki dunia papo hapo baada ya kuangukiwa na vioo vya madirisha na milango wakati wakifanya kazi ya kuvishusha kutoka kwenye gari kubwa la mizigo aina ya semi tela katika eneo la mkolani jijini Mwanza.
Tukio la kufariki dunia kwa vibarua hao waliofahamika kama Joachim Shija mkazi wa Igogo na mwenzake aliyetambulika kwa jina la Leonard Maige mkazi wa mabatini jijini Mwanza, limetokea hii leo majira ya saa nane mchana katika eneo la Mkolani Centre.
Kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza naibu kamishna wa polisi Ahmed Msangi akizungumza kwa njia ya simu amethibitisha kutokea kwa vifo hivyo.
Kwa mujibu wa mashuhuda, kazi ya kushusha vioo hivyo kutoka kwenye lori lenye namba za usajili T 844 CSK na tela lake lenye namba T 197 CFE linalomikiliwa na Said M. Said wa Manyoni mkoani Singida ilianza majira ya saa tano asubuhi, kazi hiyo ilikuwa inafanywa na vibarua kumi.
ITV imeshuhudia vioo vilivyokuwa vikishushwa kwa ajili ya kuingizwa kwenye stoo vikiwa vimevunjika vipande vipande baada ya semi tela hiyo kutikiswa na kuhama kwenye jiwe lililokuwa limeshikilia stendi yake.
Post a Comment