Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema hawezi kufika mbele ya Kamati ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge kuhojiwa kwa kuwa hajapokea barua ya kuitwa.
Makonda jana alisema hatoweza kwenda mbele ya kamati hiyo bila barua rasmi iliyomtaka kufanya hivyo.
Bunge lililokuwa likiendelea na vikao vyake Dodoma kabla ya kuahirishwa juzi, lilipitisha uamuzi wa kuwataka Makonda na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alaxander Mnyeti, kufika mbele ya kamati hiyo na kuhojiwa kutokana na kauli walizozitoa, zinazodaiwa kuudharau mhimili huo wa dola.
Lakini Makonda alisema jana “hilo suala la mimi kuitwa kwenye kamati nalisikia na kulisoma kwenye magazeti."
"Sina uhakika ni lini wamefikia uamuzi huu wa kuniita na hata kama wamefikia uamuzi huo, sijaletewa barua rasmi.”
Baada ya Bunge kupitisha uamuzi huo wa kuitaka Ofisi ya Bunge iwaandikie barua viongozi hao, juzi baadhi ya wabunge walihoji kauli ya Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, kwamba azimio la chombo hicho cha kutunga sheria kumtaka Makonda kufika mbele ya kamati kujieleza kuhusu tuhuma za kuudharau mhimili huo, halikufuata utaratibu.
Hatua hiyo iliamsha hasira kwa baadhi ya Wabunge na kuomba mwongozo kuhoji kwa nini Katibu wa Bunge ametoa kauli ambayo inakinzana na makubaliano ya Bunge.
Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara na mwezake wa Iringa Mjini Mchungaji Peter Msigwa (wote Chadema) walihoji kuhusu kauli ya Dk. Kashililah.
Waitara alisema, “Asubuhi ya leo ( juzi) nimetumiwa ‘clip’ ya sauti ya Katibu wa Bunge akikosoa uamuzi wetu hapa na pia gazeti la Habari Leo, Ukurasa wa 25, kuna habari imeandikwa.
"Katika taarifa hii, Katibu wa Bunge anasema maazimio ya Bunge yalikosewa na hayakufuata utaratibu,”alisema na kuongeza kuwa: “ Kwa maana nyingine, hatatekeleza kile tulichokubaliana.”
Mchungaji Msigwa wakati akichangia taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, alieleza kuwa hajafurahishwa na kauli ya Katibu wa Bunge.
Alisema Katibu wa Bunge amekosea kwenda katika vyombo vya habari na kudai chombo hicho cha kutunga sheria kimekosea kwa kuwa anafanya kazi ya Bunge na kwamba hajaajiri wabunge na anapaswa kufuata maagizo yao.
Hoja ya kutaka kina Makonda washughulikiwe iliwasilishwa na Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema) katikati ya wiki na ilijadiliwa na kuungwa mkono na wabunge wote, wakiwamo mawaziri kwa kusema ‘ndiyo’.
Akiwasilisha hoja hiyo kipindi cha usiku baada ya kipindi cha asubuhi kutoruhusiwa na Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge, Waitara alisema: “Haya mambo ndiyo yamejirudia wakati nikiangalia televisheni ya Clouds, Makonda akionekana akisema sisi humu bungeni tunasinzia.”
Alibainisha kuwa kwa mujibu wa Katiba ibara ya 63 (2), Bunge ndicho chombo kikuu kwa niaba ya wananchi katika kuisimamia na kuishauri Serikali na linapitisha bajeti inayotumiwa na wateule hao wa Rais.
Alisema si sawa kwa wakuu wa mikoa na wilaya kuwaweka rumande wabunge, madiwani na watumishi wa serikali.
“Bunge linaingia katika majaribu makubwa ya kudharauliwa. Tunakula kiapo humu, tunaamua kwa niaba ya Watanzania, lakini Mkuu wa Wilaya anasema hawa ni wapuuzi na Mkuu wa Mkoa anasema hawa wanalala tu.”
Baada ya hoja hiyo, Waitara alitaka ijadiliwe na Bunge na kutoa maazimio ili kurejesha heshima ya chombo hicho, hoja ambayo Chenge aliipokea na kutoa nafasi kwa wabunge wanne kujadili kutokana na muda kuwa mfupi.
Mbunge wa Ulyankulu (CCM), John Kadutu, alisema: “Nimehuzunika sana wabunge tunafika mahali tunadharauliwa, halafu watu tunaangalia tu. Haya ambayo yametokea kwa Makonda na Arumeru, pia yametokea Manispaa ya Dodoma.Mkurugenzi anaongea na wabunge kama watoto.
“Nadhani hata ile sheria ya Marekani wenzetu wanaoteuliwa kwa ngazi za juu lazima wapelekwe bungeni hapa kwetu ingefaa kuletwa ili watu wa aina hii tuweze kuwamaliza hapa hapa.
"Wapo wanaodhani wako juu yetu.”
Alisema ni jambo la hatari kujenga serikali yenye kiburi na kusisitiza“unapotaka kutoa pepo halibembelezwi. Unataka kupunga majini huwezi kubembeleza.Lazima ukazane kupunga jini litoke. Hatuwezi kutoa pepo kwa lugha nyepesi nyepesi (akipunguza sauti) pepo toka, haiwezekani. Kama ni pepo tulikemee litoke.”
Ester Bulaya (Bunda Mjini–Chadema) alieleza Makonda alivyompigia simu na kutamba kushughulikia wabunge kwa kuwa yuko karibu na ‘Bwana mkubwa’, huku akisisitiza kuwa Mkuu huyo wa Mkoa hakutengenezwa kuwa kiongozi.
“Makonda alinipigia simu na kunitisha kwamba yeye yuko karibu na Bwana mkubwa, atatushughulikia wabunge.
Alisema ataanza na (Joseph Kasheku) Msukuma (Geita-CCM), Halima Mdee (Kawe-Chadema), Esther Matiko (Tarime Mjini-Chadema), Sugu (Joseph Mbilinyi-Chadema Mbeya Mjini) na (Mchungaji Peter) Msigwa (Iringa Mjini-Chadema),” alisema.
Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea alisema “Ni lazima heshima ya Bunge ilindwe kwa gharama yoyote. Makonda anawapigia simu wabunge akitaja mmoja wa mawaziri kuwa ndiye anatuma wabunge wamtukane.”
Naye Msukuma alisema haiwezekani Makonda afanye kazi ya polisi na kuhoji aliko Mkuu wa Jeshi la Polisi, makamanda na makamishna wake.
“Makonda ni nani katika hii nchi? Kama (David) Jairo (aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini) alitoka kwa azimio la Bunge, Makonda ni nani? Mimi niko tayari kupambana na Makonda,” alisema Msukuma.
Hoja hiyo pia ilitolewa ufafanuzi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, Kazi, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, wakitaka wahusika hao wasikilizwe kwanza na kuachia ngazi zingine iwapo watabainika kutenda kosa.
Baada ya wabunge kuchangia, Chenge alitoa nafasi kwa Waitara ambaye alihitimisha hoja hiyo na kutoa maazimio manne ambayo Mwenyekiti huyo wa Bunge aliyafafanua na kupitishwa.
Maazimio hayo ni pamoja na Makonda na Mnyeti kuitwa mbele ya Kamati ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge ili kuhojiwa juu ya kauli zao zenye mwonekano wa udhalilishaji kwa Bunge, ambalo ni mhimili pacha na ule wa utawala wanaoutumikia.
Lingine ni kumtaka Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene, kutoa maelekezo kwa wakuu wa mikoa na wilaya kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na kutoingilia majukumu yasiyowahusu.
Post a Comment