Utata Mtupu ‘Dili’ Minofu ya Punda,Kasi Uchinjaji Yafika 100 kwa Siku,...!!!


UTATA umeibuka kuhusiana na biashara ya minofu ya punda nchini baada ya watetezi wa haki za wanyama kudai kuwa viumbe hao watatoweka nchini ndani ya miaka michache ijayo ikiwa kasi ya kuchinjwa kila uchao itaendelea kama ilivyo sasa.

Aidha, imeelezwa kuwa endapo jitihada hazitafanywa katika kusimamia biashara ya minofu ya wanyama hao, kuna uwezekano mkubwa wa kuongezeka kwa umaskini katika kaya za maeneo yanayotumia wanyama hao kama chombo chao cha usafiri.

Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la Ustawi wa Wanyama Tanzania (Taweso), Dk. Thomas Kahema, ndiye aliyeeleza kuhusu dalili za kutoweka kwa punda nchini wakati akizungumza katika uzinduzi wa ripoti ya biashara ya punda wilayani Mpwapwa, mkoa wa Dodoma, jana.

Mkurugenzi Msaidizi Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Joram Mghwira, ambaye anashughulikia wanyama, alikiri kuwapo kwa hatari ya kutoweka kwa punda na jambo hilo kuwaathiri wananchi wanaowatumia wanyama hao kama chombo cha kazi na usafiri, chanzo cha tishio hilo kikiwa ni pamoja na kuwapo kwa wizi na uchinjaji holela wa wanyama hao kwenye viwanda vilivyopo Dodoma na Shinyanga.

UTATA WENYEWE

Akifafanua juu ya kuwapo kwa hofu ya kutoweka kwa punda nchini, Dk. Kahema alisema kuwa hadi sasa, utafiti uliofanywa na shirika lake unaonyesha kuwa nchi nzima ina punda takribani 500,000 huku kasi ya uchinjwaji wa wanyama hao ikifikia wastani wa punda 100 kila uchao.

Alisema takwimu hizo ndizo zinazoongeza hofu ya kutoweka kwa punda na hivyo akazitaka mamlaka husika kuchukua hatua ya kusimamia sheria kwa umakini ili kuwaokoa viumbe hao.

Dk. Kahema alisema kushamiri kwa biashara hiyo kila siku, kutasababisha pia kupungua kwa nguvu kazi ya jamii zenye punda ambao huwasaidia katika shughuli zao zikiwamo za ubebaji wa mizigo na kazi nyingine mbalimbali.

Alisema mbali na biashara ya kitoweo, pia ngozi za punda zaidi ya 100 wanaochinjwa kila uchao huuzwa katika viwanda vya Wachina vilivyopo Dodoma na Shinyanga.

Aliongeza kuwa iwapo jitihada za makusudi hazitachukuliwa sasa, taifa litakuwa halina mnyama huyo kutokana na ukweli kuwa biashara ya ngozi yake pia ingali ikishika kasi kubwa China na kwingineko barani Asia.

Alisema hatari zaidi ya kutoweka kwa punda nchini inaongezwa pia na ukweli kuwa hakuna uwiano mzuri kati ya idadi ya wale wanaochinjwa kila uchao na kuzaliana kwao.

Kuhusiana na athari za kiuchumi, Dk. Kahema alisema wastani wa bei ya punda mmoja kwa sasa ni Sh. 200,000, lakini utafiti unaonyesha kuwa thamani yake kwa ujumla kutokana na mchango wake kwa kaya zenye wanyama hao ni takribani Sh. milioni 5 kwa mwaka.

“Kwa sasa punda mmoja anauzwa Sh. 200,000 wakati kwa mwaka mnyama huyo hufanya kazi ya zaidi ya Sh. milioni 5 kwa mkulima iwapo atatumika kusaidia shughuli za kulima, kuchota maji, kubeba mizigo na kazi nyingine za kila siku,” alisema Dk. Kahema.

Akizungumzia utata kuhusiana na hatima ya punda nchini, Dk. Mgwira wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, alisema pamoja na serikali kuwapa vibali wawekezaji kufungua viwanda vya nyama za punda, lakini sheria zinawataka wawekezaji hao kuwa na mikakati ya inayoonyesha jinsi watakavyoongeza kuzaliana kwa wanyama hao nchini.

Ofisa mmojawapo wa Kiwanda cha Nyama ya Punda cha Huwa Cheng Company Limited kilichopo mjini Dodoma, Mohamed Hamis, alisema baada ya kufungiwa na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na kutozwa faini kutokana na kasoro za kimazingira, sasa kiwanda hicho kimefunguliwa na kinaendelea na uzalishaji.

“Hivi sasa kwa siku tunaingiza punda 40 kulingana na kibali tulichopewa… lakini uwezo wetu ni kuchukua punda 600,”alisema Hamis, na kuongeza kuwa jana serikali iliwapatia kibali kingine cha kuingiza punda 80 kwa siku kutokana na wingi wa punda mnadani.

Kuhusu mkakati wa kuufanya uzalishaji uwe endelevu ili punda wasipotee, Hamisi alisema kuna shamba la punda mkoani Singida na hadi sasa wapo punda zaidi ya 200 wanaofugwa kukidhi sharti hilo.

Mmoja wa wafanyabiashara wa punda katika Manispaa ya Dodoma, Mussa Charles, alisema wamekuwa wakiuza punda mmoja kwa Sh. 190,000.

Visit website

Post a Comment

[blogger]

Author Name

{picture#YOUR_PROFILE_PICTURE_URL} YOUR_PROFILE_DESCRIPTION {facebook#https://fb.com/} {twitter#YOUR_SOCIAL_PROFILE_URL} {google#YOUR_SOCIAL_PROFILE_URL} {pinterest#YOUR_SOCIAL_PROFILE_URL} {youtube#YOUR_SOCIAL_PROFILE_URL} {instagram#YOUR_SOCIAL_PROFILE_URL}

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.