TUKIO la kushangaza lililohusishwa na kifo cha Denis Komba (24) baada ya nyoka aliyekuwa naye kuuawa, limechukua sura mpya baada ya mambo kadhaa kuibuka.
Hayo ni pamoja na familia kudai mzoga wa nyoka na kwenda nao kuuzika nyumbani, jambo lililoendelea kuhusisha suala hilo na imani za kishirikina.
Imeelezwa kuwa familia ilielezwa na mganga wa kienyeji kuwa mwili uliohifadhiwa hospitali, si wa mtoto wao, jambo lililowafanya kuuchukua mzoga wa nyoka na kwenda kuuweka katika mfuko wa sarandusi (kiroba) na kuuzika.
Hata hivyo, mashuhuda walieleza kuwa, familia hiyo ilikikata kichwa cha nyoka na kukizika kivyake na kiwiliwili sehemu nyingine huku mwili wa Komba ambaye naye alizikwa jana, ukizikwa katika kaburi eneo lingine tofauti. Tukio hilo ni la juzi na lilimhusu Komba, mkazi wa Mateka, manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.
Nyumbani kwao ni kilometa tano kutoka katikati ya mji wa Songea. Kabla ya maziko, baadhi ya vijana waliokuwa wamebeba jeneza, walikuwa wakikimbia nalo mwendo wa mchakamchaka huku wakiimba “mkimbize mkimbize nyoka awahi asije kudhuru watu wengine”. Katika maziko hayo, hakuna ndugu aliyeonekana kulia wala hakukuwa na ibada yoyote wakati jina la marehemu linadhihirisha kuwa ni wa imani ya Kikristo. Wakati hayo yakiendelea msibani, baadhi ya watu wake wa karibu walidai alikuwa na tabia ya kucheza na nyoka mara kwa mara.
Hata hivyo, baba mzazi alikana kumuona mwanawe na nyoka. Naye daktari aliyechunguza mwili, alisema kifo cha Komba kinatokana na kugongwa na nyoka mwenye sumu kali, lakini hakuna jeraha wala alama yoyote iliyoonekana katika mwili huo. #HabariLeo
Post a Comment