WANANCHI wa kijiji cha Kanyama kata ya Kisesa wilayani Magu mkoani Mwanza, wamecharuka na kumpa Hadija Nyembo Mkuu wa Wilaya hiyo siku 21 ili kuhakikisha anatatua mgogoro wa ardhi wa mlima Kanyama, uliodumu kwa miaka mitatu kabla hawajachukua hatua zingine, anaandika Moses Mseti.
Wananchi hao wamefikia hatua hiyo baada ya kuwepo mgogoro wa ardhi katika mlima Kanyama uliodumu kwa kipindi cha miaka mitatu sasa na kusababisha machafuko ndani ya jamii hiyo.
Mgogoro huo ulishika kasi na kufukuta zaidi mwaka 2012, ambapo ulisababisha Clement Mabina aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mwanza enzi hizo kuuwawa na wananchi wenye hasira kali.
Mabina alifikwa na umauti huo tarehe 15 Desemba, 2013 baada ya kudaiwa kuanza ujenzi katika mlima huo ambapo wananchi walifika na kuhoji sababu za yeye kuanza ujenzi hata hivyo walitoafautiana kauli na Mabina kudaiwa kurusha risasi na kumuua mtu mmoja.
Baada ya kitendo hicho wananchi walimkimbiza na kumshambulia kwa mawe, marungu na mapanga na hatimaye kumsababisha umauti papo hapo.
Wakizungumza na MwanaHALISI Online wanannchi wa eneo hilo wamesema kuwa DC Khadija asipotatua mgogoro huo kwa muda wa wiki tatu kuanzia sasa watachukua hatua nyingine za makusudi ili kutatua mgogoro huo.
Wamesema kuwa hatua hizo ni pamoja na kuwashitaki viongozi wa mkoa huo kwa William Lukuvi, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi ili aweze kuwasaidia kutatua mgogoro huo, kwani unaonekana kutishia amani.
Yohana Gervas, Mwenyekiti wa kijiji cha Kanyama, “Wananchi tunataka kujenga ofisi ya kijiji ni jambo ambalo haliwezekani eneo lipo lakini wao waendelee kufanyia kazi majumbani mwao.”
Amesema wananchi wengi wa kijiji hicho, wamekuwa wakiponda mawe na kuyauza ili kusomesha watoto wao na kujiinua kiuchumi hivyo wanaziomba mamlaka za juu kuingilia suala hilo.
“Marehemu Mabina aliwalaghai baadhi ya Wananchi na viongozi wa kijiji, kwamba angewajengea darasa moja la shule ya msingi Kanyama na visima vitatu vya maji ambavyo hata hivyo hakutekeleza ahadi hiyo mpaka leo,” amesema.
Hata hivyo Khadija Nyembo Mkuu wa wilaya hiyo, amewataka wananchi hao kuvuta subira huku akidai kwamba ifikapo Januari 27, 2017 suala hilo atakuwa amelipatia ufumbuzi.
Post a Comment