Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, amepiga marufuku usafirishaji wa mchanga wa madini nje ya nchi na ametaka mchanga wote ufanyiwe uyeyushaji hapa hapa nchini.
Rais Magufuli ametoa katazo hilo leo wakati akiweka jiwe la msingi la kiwanda cha kutengeneza vigae (Tiles) cha Kampuni ya Goodwill Tanzania Ceramic Limited kilichopo katika Wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani.
Akizungumza baada ya kutembelea kiwanda hicho, Mhe. Rais Magufuli ameishukuru Menejimenti ya kiwanda hicho kwa uwekezaji huo na ameelezea kufurahishwa kwake na kutumika kwa teknolojia ya kuyeyusha mchanga wa kutengenezea vigae.
"Nchi hii tumechezewa vya kutosha, sasa nyinyi hapa mnayeyusha mchanga kwa kuuchemsha hadi nyuzi joto 1,000 wakati wengine wanasafirisha mchanga nje ya nchi wakati uchemshaji wake hauhitaji kufika hata nyuzi joto 1,000, naiagiza Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji na Wizara ya Nishati na Madini kuwa kuanzia sasa ni marufuku kusafirisha mchanga nje ya nchi" amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Kiwanda hicho kikubwa Afrika Mashariki na Kati ambacho ujenzi wake umegharimu Dola za Marekani Milioni 50 kwa awamu ya kwanza kitakuwa na uwezo wa kuzalisha mita za mraba 80,000 za vigae kwa siku, kitazalisha ajira za moja kwa moja 1,000 na ajira zisizo za moja kwa moja 2,000.
Akizungumza kabla ya kuweka jiwe la msingi la kiwanda hicho Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na uwekezaji Dkt. Adelhelm Meru amesema pamoja na kiwanda hicho, tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani jumla ya viwanda 2,169 vinavyojumuisha viwanda vidogo, vya kati na vikubwa vimesajiliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na vipo katika hatua mbalimbali za kukamilika.
Naye Balozi wa China hapa nchini Mhe. Dkt. Lu Youqing amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa kutilia mkazo juhudi za kukuza uchumi zilizowezesha Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zenye uchumi unaokuwa kwa kasi kubwa Barani Afrika na amebainisha kuwa China itaendelea kushirikiana na Tanzania kuendeleza uwekezaji nchini Tanzania ikiwemo kujenga viwanda.
"Mhe. Rais kwa mujibu wa takwimu za TIC mpaka mwisho wa Juni 2016 uwekezaji wa moja kwa moja kutoka China umefikia Dola za Marekani Bilioni 6.6 na umezalisha ajira za moja kwa moja kwa Watanzania 150,000 na zisizo za moja kwa moja 450,000 na kiwanda hiki cha Goodwill Tanzania Ceramic Limited kimejengwa na wawekezaji kutoka China, vipo viwanda vingine vingi vinajengwa, Mbunge wa Mkuranga ameniambia kuwa kuna viwanda zaidi ya 50 vya Wachina vinavyojengwa hapa Mkuranga, nimefurahi sana kuona karibu kila sekta Watanzania wanafurahia ushirikiano wa Tanzania na China" Amesema Balozi Dkt. Lu Youqing.
Post a Comment