Kikosi cha usimamizi wa rasilimali za uvuvi kanda ya Mwanza kwa kushirikiana na jeshi la polisi mkoani Mwanza, kimekamata watuhumiwa 14 wa uvuvi haramu, wakiwa na nyavu 1,660 za Makila, Makokoro matano ya Sangara, mitumbwi 8 na injini 7 za mitumbwi katika doria iliyofanyika usiku wa kuamkia leo.
Afisa mfawidhi wa usimamizi wa raslimali za uvuvi kanda ya Mwanza Lameck Mongo amesema doria hiyo imefanyika katika kisiwa cha Makobe kilichomo ndani ya ziwa Victoria, ikiwa ni mwendelezo wa vita dhidi ya uvuvi haramu.
Mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai mkoa wa Mwanza kamishna msaidizi wa polisi ACP Augustino Senga amesema watuhumiwa hao 14 waliokamatwa na zana hizo haramu za uvuvi watafikishwa mahakamani baada ya kuchukuliwa maelezo yao.
Msako dhidi ya uvuvi haramu unakuja wakati wavuvi wa mikoa ya Mara, Kagera, Simiyu na Mwanza wakiwa katika mgomo usiokuwa na kikomo kutokana na kupinga agizo la waziri wa kilimo, mifugo na uvuvi Dk. Charles Tizeba alilolitoa Januari 24 mwaka huu jijini Mwanza, la kuwataka kutumia nyavu zenye matundu 26, ambazo ni mwafaka kwa uvuvi endelevu badala ya nyavu zenye matundu 78 ambayo wanadai yamekuwa yakitumika tangu biashara ya usindikaji wa minofu ya Sangara viwandani ilipoanza mwanzoni mwa miaka ya 2000.
Post a Comment